Ufadhili Mdogo Kutoka Shirika la OMDTZ — 2021

OpenMap Development Tanzania
3 min readApr 6, 2021

By Hawa Adinani

Muda wa kutuma maombi umeongezwa hadi tarehe 31, Mei 2021

Ukihitaji kuwasilisha maombi kwa lugha ya kiingereza bofya hapa

Shirika la OpenMap Development Tanzania kwa kushirikiana na Humanitarian OpenStreetMap Team (HOT) kupitia mradi wa ‘Audacious Project’ wanakusudia kusaidia jamii za OpenStreetMap (ramani ya mtandaoni ya wazi kabisa ambayo kila mmoja anaweza kuongeza na kurekebisha taarifa zilizopo) kupitia ufadhili mdogo wa miradi utakaotolewa na OMDTZ. Huu ni mpango wa msaada kwa jamii za wenyeji nchini Tanzania (bara na visiwani) kuweza kutumia data za OSM na zana nyinginezo kusaidia kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii zao kupitia data. OMDTZ inakusudia kufadhili miradi na/au jamii ambazo zinaleta mabadiliko ya muktadha wa eneo, na maoni ya vitendo kutoka ngazi ya chini ambayo inakusudia kutatua shida za jamii kupitia ramani.

Ufadhili huu mdogo unakusudia kutoa kiasi cha shilingi za kitanzania 5,750,000/= hadi 11,500,000/= kwa kila moja kwa angalau jamii/taasisi nane (8) zinazojihusisha au zitakazojihusisha na OSM kote Tanzania na yenye mawazo ya kiutendaji juu ya jinsi data za OSM na ramani zitavyosaidia jamii zao kutatua changamoto maalum na kuleta suluhisho chanya na endelevu.

Madhumuni ya ufadhili huu ni kuongeza na kupanua ushiriki wa jamii ya Tanzania katika utengenezaji wa ramani huru na za wazi kama rasilimali muhimu wanayohitaji kukua na kuchangia suluhisho la changamoto zinazoathiri maisha yao ya kila siku. OMDTZ inatarajia kuwa hii itapelekea maendeleo katika shughuli za kijamii na kiuchumi na masuala mengine ambayo yanategemea data zilizopo wazi.

Miradi itakayowasilishwa lazima iwe sambamba na kanuni zifuatazo:

  • Malengo wazi ya mradi: maombi yatakayofanikiwa yatafafanua wazi malengo ya mradi na kubainisha lengo kuu la mradi utakapokamilika, orodha ya shughuli na jinsi zitakavyofanyika, utekelezaji wa shughuli za kila siku, uhusishwaji wa jamii, na maono ya mbali ya matokeo ya mradi.
  • Umilikishwaji: maombi yatakayofanikiwa yatalazimika kuonyesha jinsi jamii au shirika litavyomiliki data/taarifa zilizokusanywa, jinsi watakavyotumia kutatua changamoto zinazowakabili, ni nani anayehitaji data au mafunzo yatakayotolewa, na kwanini. Kipaumbele kitapewa kwa miradi ambayo itazingatia sana kutatua na kuonyesha shida na changamoto za jamii.
  • Ujumuishwaji: kuzingatia jinsia, kujumuishwa kwa vijana na vikundi vilivyotengwa/ visivyopewa fursa nyingi (marginalised groups). Kipaumbele kitapewa kwa maombi ambayo yanajumuisha na kujengea ujuzi wanawake na watoto katika mafunzo ya zana huru za utengenezaji ramani na ukusanyaji wa taarifa. Lengo ni kuongeza idadi ya wanawake na vikundi vingine vilivyotengwa kujifunza na kutumia zana na vifaa mbalimbali kukuza uwezo wao na kujihusisha katika kutatua changamoto za jamii.
  • Mapinduzi ya ujuzi huria: Kipaumbele kitapewa miradi ambayo inakusudia kufikia maeneo ya pembezoni mwa nchi ili kuongeza na kufundisha jamii juu ya mfumo wa OSM. Pia, kipaumbele kitapewa kwa miradi na maombi yenye mpango wa kuongeza jamii mpya za OSM na kusaidia ukuaji wake katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
  • Ushirikiano: Kipaumbele kitapewa kwa miradi ambayo itafanya kazi pamoja kama washirika au kutengeneza ushirikiano baina yao na serikali za mitaa, sekta binafsi au mashirika ya jamii ili kupata wataalamu au mabingwa (champions) wa masuala ya OSM na utengenezaji wa ramani hata baada ya muda wa ufadhili kufikia ukomo. Hii itasaidia katika kurahisisha kazi zao kwa kutumia tecknologia na data zilizokusanywa

Maelezo kuhusu wanaostahili kupata ufadhili yanapatikana hapa.

Jinsi ya kutuma maombi

Ili kuwasilisha ombi lako, lazima ujaze fomu hii na maelezo yote ya maombi yanayohitajika. Tumia mfano huu wa mpango wa mradi na mfano huu wa bajeti ya mradi. Maombi yote yatahitaji kuzingatia kwa uangalifu kanuni tano za mradi zilizoainishwa hapo juu. Ikiwa unahitaji msaada wowote, tafadhali wasiliana na asha.mustapha@hotosm.org.

Muda wa kutuma maombi umeongezwa hadi tarehe 31 Mei 2021.

Msaada wa Kuandaa Mradi (Mentoring)

Ushauri utapatikana kwa waombaji wote kwa mwezi mmoja (1) kabla ya uwasilishaji ambao utajumuisha msaada katika maoni ya mradi, upangaji wa mradi, uundaji wa bajeti, na ushauri juu ya ushiriki wa wadau. Tutatoa ushauri kwa waombaji wote ili tuweze kusaidia jamii ambazo zina mawazo (idea) mazuri ya mradi ya kutatua changamoto za jamii lakini haziwezi kuunda mawazo yao kwa mfumo mzuri wa maandishi ili kuweza kupata ufadhili.

Kila mwombaji atakaekuwa na nia ni lazima aombe mshauri ambaye atawasaidia kupitia mchakato mzima wa maombi. Unaweza kuomba mshauri kwa kutuma ombi lako kupitia barua pepe asha.mustapha@hotosm.org ikiambatana na jina la mradi wako.

Kumbuka: Maombi yatayokubaliwa ni ya Tanzania tu (bara na visiwani). Maombi nje ya Tanzania hayatakubaliwa.

--

--

OpenMap Development Tanzania

Open-source tech & geodata for managing & solving community's socio-economic and humanitarian challenges